Vikao Vya Kamati za Bodi ya Wakurugenzi
Mwenyekiti wa Kamati ya Bodi ya Ukaguzi na Usimamizi wa Vihatarishi COASCO Aipongeza Menejimenti ya Shirika kwa Kuleta Mabadiliko na Ufanisi katika Kazi Zake
Kamati mbalimbali zimefanya vikao kama maandalizi ya kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa COASCO, ambacho kitafanyika tarehe 21 Agosti 2025.
Katika vikao hivyo, Kamati ya Ukaguzi na Usimamizi wa Vihatarishi ya Bodi ya COASCO imefanya kikao tarehe 18.08.2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Shirika uliopo Jijini Dodoma.
Kikao hicho kimepitia miongozo na sera mbalimbali za Shirika pamoja na kujadili utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Mkaguzi wa ndani pamoja na Mkaguzi wa nje.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, CPA Aziz Dachi, kimetoa maelekezo kwa Menejimenti ya Shirika kuhakikisha kuwa mapendekezo yote yafanyiwe kazi pamoja na kuboresha sera na miongozo iliyowasilishwa kulingana na sheria na kanuni zilizopo.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bodi ya Mipango na Uchumi, Bi. Consolata Kiluma, ametoa wito wa kudumisha ushirikiano kati ya Shirika na wadau wote ili kuleta umoja, ufanisi na tija katika kazi zetu.
Aidha, katika kuhitimisha vikao hivyo, Wenyekiti wa Kamati wamemshukuru Menejimenti kwa jinsi wanavyosimamia shughuli za Shirika, ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuleta mageuzi ya kiutendaji na kuongeza ufanisi katika kazi zinazofanywa na Shirika.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika, CPA Jeremiah J. Mugeta, amewashukuru Wenyekiti na Wajumbe wote kwa jinsi walivyosimamia vikao vya kamati zao. Pia amepokea mapendekezo yote na ameahidi kuyafanyia kazi yote waliyoelekeza kwenye vikao hivyo.