COASCO YASHIRIKI MAADHIMISHO YA KIMATAIFA YA SIKU YA USHIRIKA WA AKIBA NA MIKOPO ULIMWENGUNI – ICUD 2025 JIJINI ARUSHA
COASCO YASHIRIKI MAADHIMISHO YA KIMATAIFA YA SIKU YA USHIRIKA WA AKIBA NA MIKOPO ULIMWENGUNI – ICUD 2025 JIJINI ARUSHA
Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limeungana na wadau mbalimbali wa sekta ya ushirika kushiriki katika Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Ushirika wa Akiba na Mikopo Duniani (International Credit Union Day – ICUD 2025) yanayofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 30 Septemba hadi 02 Oktoba 2025.
Maadhimisho haya ni fursa muhimu ya kimataifa inayowakutanisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa vyama vya akiba na mikopo, kubadilishana uzoefu na mbinu bora za usimamizi na ukaguzi, pamoja na kujadili nafasi ya vyama vya ushirika katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kupitia ushiriki wake, COASCO inasisitiza dhamira yake ya kuhakikisha vyama vya ushirika vinaendeshwa kwa uwazi, uwajibikaji na kufuata misingi ya usimamizi bora wa fedha. Pia, ni fursa ya kujifunza mbinu za kisasa za ukaguzi na usimamizi ambazo zitasaidia kuimarisha ustawi wa vyama vya akiba na mikopo nchini.
Kauli mbiu ikiwa ni “Ushirikiano kwa Ulimwengu wenye Ustawi.”
Kauli mbiu hii inakumbusha umuhimu wa Mshikamano na Ushirikiano wa vyama vya ushirika katika kujenga jamii zenye Ushirikiano, Ustawi na Maendeleo endelevu.
Kwa kushirikiana na wadau wengine, COASCO itaendelea kuwa chachu ya kuhakikisha sekta ya ushirika inabaki kuwa chombo madhubuti cha kujenga maisha bora ya wanachama na jamii kwa ujumla.