Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO)

COASO Logo
MAONESHO YA NANENANE 2024, KITAIFA KUFANYIKA MKOANI DODOMA
08 Aug, 2024 06:00AM-06:00PM
Dodoma
mrisho.rashid@coasco.go.tz

Wizara ya Kilimo imewafahamisha wananchi na wadau wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuwa Maadhimisho na Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nane Nane) Kitaifa yatafanyika  jijini Dodoma kuanzia tarehe 1 - 8 Agosti, 2024. 

Akizungumza na waandishi wa Habari tarehe 4 Juni 2024 jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb), amesema maonesho hayo yataendelea kuwa ya Kimataifa ambapo tayari baadhi ya nchi jirani zimethibitisha kushiriki katika maonesho hayo.

Ameongeza kuwa kampuni mbalimbali zinazonunua na kuuza bidhaa za kilimo zitashiriki katika kanda saba (7) ambazo ni Kanda ya Nyanda za Juu Kusini jijini Mbeya  kwenye uwanja wa John Mwakangale; Kanda ya Mashariki mjini Morogoro kwenye viwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere; Kanda ya Kusini mjini Lindi kwenye viwanja vya Ngongo; Kanda ya Ziwa Magharibi jijini Mwanza katika viwanja vya Nyamhongolo; Kanda ya Ziwa Mashariki  mkoani Simiyu katika viwanja vya Nyakabindi; Kanda ya Kaskazini jijini Arusha kwenye viwanja vya Themi; na Kanda ya Magharibi mjini Tabora kwenye viwanja vya Fatma Mwasa. 

Aidha, Serikali imeanza ujenzi wa uwanja wa  maonesho Nanenane jijini Dodoma ili uwe na ubora wa kimataifa ambapo kwa awamu ya kwanza ujenzi wake utagharimu shilingi bilioni 7.5.

Waziri Bashe ameongeza kuwa kuhusu ujenzi wa John Mwakangale jijini Mbeya tayari zabuni  imeshatangazwa ili kumpata mkandarasi atakayejenga uwanja huo. Ujenzi wa viwanja hivyo utahusisha ujenzi wa barabara za ndani ya kiwanja, ujenzi wa ukuta wa eneo lote la kiwanja, pamoja eneo maalumu la maonesho, kumbi za mikutano,  mifumo ya maji na mashamba yatakayotumika kwa ajili ya mafunzo kwa muda wa mwaka mzima.

Mgeni rasmi tarehe 1 Agosti 2024 wakati wa ufunguzi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango na siku ya kilele itakuwa tarehe 8 Agosti 2024 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kauli Mbiu ya Maonesho ni “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”.

MAONESHO YA NANENANE 2024, KITAIFA KUFANYIKA MKOANI DODOMA