Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO)

COASO Logo
WATUMISHI WAPYA 10 WA COASCO WAPEWA MAFUNZO ELEKEZI YA UTUMISHI WA UMMA
07 Jun, 2026
WATUMISHI WAPYA 10 WA COASCO WAPEWA MAFUNZO ELEKEZI YA UTUMISHI WA UMMA

WATUMISHI WAPYA 10 WA COASCO WAPEWA MAFUNZO ELEKEZI YA UTUMISHI WA UMMA

Watumishi wapya 10 wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) wamepewa mafunzo elekezi ya utumishi wa umma kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu maadili, sheria, kanuni, taratibu na utoaji wa huduma bora katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mafunzo hayo yamefunguliwa Juni 4, 2026 katika Ukumbi wa Maktaba wa Ofisi ya Mkoa wa Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COASCO, CPA Jeremiah Mugeta, ambaye amewapongeza na kuwakaribisha watumishi hao ambao ni Wakaguzi, Afisa tehema, Afisa uhusiano wa umma na maafisa usafirishaji katika Shirika.

“Ninaamini mafunzo haya elekezi yatawawezesha kupata uelewa wa kutosha kuhusu sheria, miiko, kanuni na taratibu za utumishi wa umma pamoja na kuifahamu vyema utamaduni wa Shirika,” amesema CPA Mugeta.

Aidha, CPA Mugeta amewasisitiza watumishi hao kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kuwa waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao na kuepuka vitendo vya rushwa ili kulinda heshima ya utumishi wa umma na ya Shirika kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa COASCO, CPA Prisilla Mushi, amesema anaamini mafunzo hayo yatawawezesha watumishi hao kuanza majukumu yao wakiwa na uelewa sahihi wa maadili, taratibu za kazi na utamaduni wa Shirika, jambo litakalochangia kuongeza ufanisi katika utendaji wao.

Naye Anderson Mbiaji, kwa niaba ya watumishi wenzake, ameishukuru Menejimenti ya COASCO kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa yatawasaidia kuongeza maarifa, uwezo na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.