BODI YA WAKURUGENZI COASCO YASISITIZA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA UKAGUZI KWA VYAMA VYA USHIRIKA
BODI YA WAKURUGENZI COASCO YASISITIZA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA UKAGUZI KWA VYAMA VYA USHIRIKA
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) imefanya kikao chake cha 86 kwa lengo la kupokea, kujadili na kuchambua taarifa mbalimbali ya kiutendaji ikiwemo ukaguzi, usimamizi wa vihatarishi, uchumi, mipango, ajira, maendeleo ya utumishi na utawala ili kuzidi kuimarisha utendaji wa Shirika na kuboresha zaidi huduma za ukaguzi na usimamizi kwa vyama hivyo.
Akiongoza kikao hicho leo Juni 11, 2026 kilichofanyika katika Ukumbi wa PSSSF, Dodoma, Mwenyekiti wa Bodi ya COASCO, CPA Juma A. Kimori, ambaye alishiriki kikao hicho kwa njia ya mtandao, amesisitiza Menejimenti kuendelea kutekeleza kwa wakati maelekezo na maamuzi ya Bodi ili kuboresha huduma za ukaguzi kwa vyama vya ushirika nchini.
CPA Kimori amesema kikao hicho kimejikita katika kupitia utekelezaji wa majukumu ya Shirika na kutathmini maendeleo yake, ambapo Bodi pia imeidhinisha masuala mbalimbali ya kiutendaji ikiwemo bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 pamoja na Mpango wa Manunuzi wa mwaka 2026/2027.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COASCO, CPA Jeremiah Mugeta, amesema Menejimenti itaendelea kutekeleza maelekezo yote ya Bodi na Serikali kwa wakati ili kuzidi kuimarisha utendaji wa Shirika.
