MADEREVA COASCO WAPATIWA MAFUNZO MAALUM, KUONGEZA UFANISI WA UTENDAJI
MADEREVA COASCO WAPATIWA MAFUNZO MAALUM, KUONGEZA UFANISI WA UTENDAJI
Madereva wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) wamepatiwa mafunzo ya matumizi sahihi ya magari ya Serikali kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwajibikaji na nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mafunzo hayo yamefunguliwa leo Februari 28, 2026 na Meneja Rasilimali watu na Utawala, Vicent Bukombe katika ukumbi wa Shirika ofisi ya Dodoma Makao Makuu, ambaye amesema mafunzo hayo yataboresha zaidi utendaji wa madereva hao.
“Katika mafunzo haya napenda kuwasisitiza madereva wote wa COASCO kuendelea kufuata sheria za Utumishi wa Umma na taratibu za usimamizi wa magari ya Serikali, pamoja na kuzingatia taratibu za utekelezaji wa e - Utendaji wanapojaza malengo na majukumu yao” amesema Bukombe
Pia, Bukombe amewataka madereva hao kutumia magari hayo kwenye matumizi sahihi ya Shirika na sio matumizi binafsi na kuwasisitiza kutochukua gari la Shirika bila kibali.
Naye, Mwenyekiti wa Madereva wa Shirika hilo, Sebastian Shao ambaye pia ni mkufunzi wa mafunzo hayo, amesema mafuzo hayo ni ya siku moja na yamehudhuriwa na jumla ya Madereva 17 Kutoka mikoa mbalimbali, huku baadhi yao wameshiriki kwa njia ya mtandao (Google meeting), mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Mshiriki wa Mafunzo hayo, Mndima Kulewa, kwa niaba ya washiriki ameushukuru Uongozi wa Shirika kwa mafunzo na wameahidi kuwa watazingatia mafunzo yote yaliyotolewa na watafanyia kazi kwa uadilifu, uwajibikaji na uzalendo kwa manufaa ya Shirika na Taifa kwa ujumla.
