COASCO YAENDESHA MAFUNZO KWA WATENDAJI WA VYAMA VYA USHIRIKA
Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limeandaa mafunzo ya siku tatu kwa Watendaji na Viongozi wa Vyama vya Ushirika pamoja na Wadau wa Ushirika yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Morena iliyopo Morogoro mjini kuanzia tarehe 25 hadi 27 Septemba 2024.
Shirika limejipanga kutoa elimu kuhusu masuala ya Uhasibu na Mifumo ya TEHAMA na yanaratibiwa na Wataalam mbalimbali kutoka COASCO.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala CPA Prisilla Mushi amesema
“Lengo la Mafunzo haya, kwanza nikuwajengea uwezo Watendaji, Viongozi na wadau wa Ushirika ambao ndio wamekuwa wadau wakuu wa Ushirika na kuhakikisha shughuli zote za Ushirika zinanufaisha Umma wa Watanzania zikiwa katika hali ya ubora kwa kutumia njia mbali mbali za utoaji taarifa, uchakataji wa taarifa, utunzaji wa kumbukumbu na shughuli nyingine mbalimbali wanazozitoa kupitia vyama vyenu vya Ushirika na vyama vinginevyo,”
CPA Mushi amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa programu za Shirika katika kuhakikisha sekta ya Ushirika inakuwa bora zaidi kuanzia kwenye uandishi wa vitabu na nyaraka mbalimbali za utunzaji wa taarifa za Vyama vya mazao (AMCOS), Vyama Vikuu(UNIONs) pamoja na Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) hadi kufikia kwenye Ukaguzi ulio na tija na hatimaye kupunguza Hati zisizo na maoni.