Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO)

COASO Logo
COASCO Yaongeza Uwajibikaji wa Vyama vya Ushirika Kupitia Ukaguzi na Mafunzo
09 Aug, 2026
COASCO Yaongeza Uwajibikaji wa Vyama vya Ushirika Kupitia Ukaguzi na Mafunzo

COASCO  Yaongeza Uwajibikaji wa Vyama vya Ushirika Kupitia Ukaguzi na Mafunzo

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika Tanzania (COASCO) limesema linaendelea kuimarisha uwajibikaji na utawala bora katika vyama vya ushirika kupitia ukaguzi wa hesabu, mafunzo na huduma za ushauri zinazolenga kulinda rasilimali za wanachama na kuongeza ufanisi wa vyama hivyo.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COASCO, CPA Jeremiah Mugeta, wakati akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea kwenye Viwanja vya John Malecela jijini Dodoma.

CPA Mugeta amesema shirika hilo lina majukumu makuu matano ambayo ni kukagua vyama vya ushirika, kutoa huduma za usimamizi na ushauri, kukagua taasisi na makampuni mengine pamoja na kutoa huduma za kitaalamu zinazochangia maendeleo ya sekta ya ushirika.
 Amewakaribisha wananchi kutembelea banda la COASCO lililopo ndani ya banda la Wizara ya Kilimo ili kujifunza huduma zinazotolewa na shirika hilo pamoja na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya ushirika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa COASCO, Prisila William Mushi, amesema mafunzo yanayotolewa kwa viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika yamechangia kuongezeka kwa hati safi za ukaguzi na kupungua kwa hati zenye dosari.

Prisila amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, vyama vilivyopata hati safi za ukaguzi vimeongezeka hadi asilimia 20 kutoka asilimia 16 mwaka 2024/2025, huku hati mbaya zikishuka kutoka asilimia 17 hadi asilimia 13. Amesema mafanikio hayo yanaonesha mchango wa mafunzo katika kuimarisha usimamizi wa fedha, utawala bora na ulinzi wa rasilimali za wanachama wa vyama vya ushirika.