Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO)

COASO Logo
COASCO, TUICO WASAINI MKATABA WA KUUNDA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA COASCO
23 Aug, 2026
COASCO, TUICO WASAINI MKATABA WA KUUNDA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA COASCO

COASCO, TUICO WASAINI MKATABA WA KUUNDA BARAZA LA WAFANYAKAZI

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limesaini mkataba na Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri Tanzania (TUICO) wa kuunda Baraza la Wafanyakazi wa Shirika hilo, kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya Menejimenti na wafanyakazi, kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyakazi pamoja na kuongeza tija na ufanisi kazini.

Mkataba huo umesainiwa leo, Agosti 20, 2026, katika kikao kilichowakutanisha Menejimenti ya COASCO na uongozi wa TUICO kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Shirika jijini Dodoma. 

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COASCO, CPA Jeremiah Mugeta, amesema Baraza hilo litakuwa jukwaa muhimu la kusikiliza kero na changamoto za wafanyakazi na kuzitafutia ufumbuzi kupitia majadiliano.

“Leo tumesaini mkataba na TUICO wa kuunda Baraza la Wafanyakazi wa COASCO, ambalo litasaidia kuweka mazingira bora na yenye tija mahali pa kazi. Kupitia vikao na majadiliano mbalimbali, Baraza hili litasaidia kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu,” amesema CPA Mugeta.

Kwa upande wake, Mkuu wa Sekta ya Huduma na Ushauri wa TUICO, Martin Wawa, amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni hatua muhimu itakayosaidia kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na kuboresha mazingira ya kazi.

Naye, Katibu wa TUICO Mkoa wa Dodoma, Messe Max Chabba, amesema baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, hatua inayofuata ni kuunda rasmi Baraza la Wafanyakazi wa COASCO kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazohusu uundaji wa mabaraza ya wafanyakazi nchini.