COASCO YASISITIZA UWASILISHAJI WA TAARIFA ZA FEDHA KWA WAKATI KWA VYAMA VYA USHIRIKA
COASCO YASISITIZA UWASILISHAJI WA TAARIFA ZA FEDHA KWA WAKATI KWA VYAMA VYA USHIRIKA
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), CPA Prisilla Mushi, amewasihi viongozi wa vyama vya ushirika kuwasilisha taarifa za fedha kwa wakati ili kuwezesha ukaguzi kufanyika kwa wakati.
CPA Prisilla ametoa rai hiyo leo, Aprili 24, 2026 jijini Morogoro, akimwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, CPA Jeremiah Mugeta, wakati wa kufunga mafunzo ya kodi, matumizi ya Excel, uandaaji wa taarifa za fedha pamoja na taarifa za uendelevu kwa watendaji wa vyama vya ushirika, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Morena.
“Baadhi ya vyama vya ushirika bado havijakamilisha na kuwasilisha taarifa za fedha ndani ya muda uliowekwa kisheria kwa ajili ya ukaguzi hivyo, napenda kuwasihi viongozi wote kuweka utaratibu madhubuti wa kuandaa na kuwasilisha taarifa hizo kwa wakati ili ukaguzi ufanyike kwa wakati,” amesema CPA Prisilla.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 55 cha Sheria ya Vyama vya Ushirika, vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) vinapaswa kuwasilisha taarifa za fedha ndani ya miezi mitatu baada ya kumalizika kwa mwaka wa fedha.
Aidha, amesisitiza kuwa maendeleo ya chama chochote yanategemea uongozi bora na uwajibikaji, hivyo ni muhimu kwa viongozi kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha, kuzingatia sheria na kulinda maslahi ya wanachama wakati wote.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Ushauri na Mafunzo wa COASCO, CPA Denis Barongo, amewashukuru washiriki 309 kwa kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo ya siku tatu, akibainisha kuwa yamewajengea uwezo na kuongeza ufanisi katika utendaji wa vyama vyao.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Emmanuel Wawa, kwa niaba ya wenzake, ameishukuru Menejimenti ya Shirika hilo kwa kuandaa mafunzo hayo yaliyolenga kuimarisha uendeshaji wa vyama vya ushirika.
