Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO)

COASO Logo
CPA MUGETA AWAHIMIZA WAKAGUZI KUTUMIA MAFUNZO YA UCHUNGUZI KUIMARISHA UTOAJI WA HUDUMA
28 May, 2026
CPA MUGETA AWAHIMIZA WAKAGUZI KUTUMIA MAFUNZO YA UCHUNGUZI KUIMARISHA UTOAJI WA HUDUMA

CPA MUGETA AWAHIMIZA WAKAGUZI KUTUMIA MAFUNZO YA UCHUNGUZI KUIMARISHA UTOAJI WA HUDUMA

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), CPA Jeremiah Mugeta, amewahimiza wakaguzi wa Shirika hilo kutumia mafunzo maalum ya uchunguzi kama chachu ya kuongeza weledi, uaminifu na ubora wa utoaji wa huduma kwa wateja.

Rai hiyo ameitoa leo, Mei 24, 2026 wakati wa kufunga mafunzo hayo ya siku tano yaliyofanyika katika Ukumbi wa Uzunguni Park jijini Dodoma.

CPA Mugeta amesema mafunzo hayo yamewaongezea washiriki maarifa kuhusu mbinu za kisasa za kufanya uchunguzi, uandishi wa ripoti za uchunguzi zenye viwango vya juu vya kitaaluma, usimamizi wa udanganyifu pamoja na uchambuzi na uchakataji wa taarifa kubwa za uchunguzi (Big Data Analytics), mambo yatakayosaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha, amewashukuru wakufunzi wote kwa kutoa mafunzo yenye tija yatakayosaidia kuboresha zaidi huduma za shirika kwa wadau, huku akiwataka washiriki kurejea kazini na kuwajengea uwezo watumishi wenzao ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji wa COASCO.

Naye, Mkaguzi wa COASCO kutoka ofisi ya Makao Makuu Dodoma CPA Laban Nyigana, kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, ameushukuru uongozi wa Shirika kwa kuwawezesha kushiriki mafunzo hayo yaliyowaongezea uelewa na uwezo wa kitaalamu katika masuala ya uchunguzi.