WATUMISHI WAPYA COASCO WAASWA KUZINGATIA WELEDI, UBUNIFU NA UADILIFU KAZINI
WATUMISHI WAPYA COASCO WAASWA KUZINGATIA WELEDI, UBUNIFU NA UADILIFU KAZINI
Watumishi wapya 10 wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) wameaswa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na uadilifu, kujenga mahusiano mazuri na wateja, kuzingatia mavazi ya utumishi wa umma na kutumia muda wa kazi ipasavyo ili kuongeza ufanisi wa Shirika.
Rai hiyo imetolewa leo Juni 5, 2026 na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa COASCO, CPA Prisilla Mushi, wakati wa kufunga mafunzo elekezi ya utumishi wa umma kwa watumishi wapya wa Shirika hilo.
CPA Mushi amewahimiza watumishi hao kutekeleza majukumu yao kwa ubunifu na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea, huku wakizingatia uadilifu na uwajibikaji ili kuleta matokeo chanya katika utendaji wa Shirika.
“Muombe Mungu, fanya kazi kwa bidii, kuwa mbunifu na muaminifu katika utekelezaji wa majukumu yako, kuwa na uhusiano mzuri na wateja, na kuzingatia mavazi yanayoruhusiwa katika utumishi wa umma,” amesema CPA Mushi.
Aidha, amewakumbusha umuhimu wa kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora ili kuimarisha afya zao, jambo litakalowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi.
Kwa upande wake, Ibrahim Mtale, kwa niaba ya watumishi wenzake, ameishukuru Menejimenti ya COASCO kwa kuandaa mafunzo hayo yaliyowaongezea uelewa kuhusu utumishi wa umma na shughuli za Shirika.
Mafunzo hayo yalianza Juni 4 na kuhitimishwa Juni 5, 2026, yakihusisha mada mbalimbali zilizowasilishwa na wakuu wa vitengo wa COASCO pamoja na wawakilishi kutoka PSSSF, TAKUKURU, TUICO, Maliwazo na ASF SACCOSS
