Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO)

COASO Logo
COASCO: MAFUNZO YAWE CHACHU YA MABADILIKO YA UTENDAJI WA VYAMA VYA USHIRIKA
26 Sep, 2026
COASCO: MAFUNZO YAWE CHACHU YA MABADILIKO YA UTENDAJI WA VYAMA VYA USHIRIKA

COASCO: MAFUNZO YAWE CHACHU YA MABADILIKO YA UTENDAJI WA VYAMA VYA USHIRIKA

Viongozi na watendaji wa Vyama vya Ushirika wameaswa kutumia maarifa waliyoyapata kupitia mafunzo ya Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) kuleta maboresho ya vitendo katika uendeshaji na utendaji wa vyama vyao.

Rai hiyo imetolewa leo, Septemba 25, 2026, na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa COASCO, CPA Jeremiah Mugeta, wakati akihitimisha mafunzo hayo katika ukumbi wa Mabeyo, jijini Dodoma, akiwataka washiriki kuhakikisha maarifa waliyoyapata yanatafsiriwa katika hatua na maboresho yanayoweza kuonekana katika uendeshaji wa Vyama vya Ushirika.

“Mafunzo pekee hayabadili utendaji wenu endapo hatutachukua hatua katika kuendesha na kusimamia Vyama vya Ushirika. Hivyo, mtumie maarifa hayo kuleta mabadiliko katika Vyama vya Ushirika,” amesema CPA Mugeta.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri na Tafiti wa COASCO, CPA Golden Kajaba, amewataka viongozi na watendaji kuzingatia miongozo na taratibu katika uendeshaji wa vyama, akieleza kuwa Kurugenzi hiyo ipo kwa ajili ya kuwasaidia katika uandaaji wa miongozo, tafiti, ushauri wa kitaalam na mafunzo. 

Naye, Mjumbe wa Bodi ya Tembo Mgwaza SACCOS, Justina Edwin Songea, kwa niaba ya washiriki, amesema mafunzo hayo yamekuwa na tija na yatawasaidia kuboresha utendaji na maendeleo ya chama chao.