Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO)

COASO Logo
WATUMISHI COASCO TANGA WAASWA KUFANYA KAZI KWA BIDII NA UADILIFU ILI KUIMARISHA HUDUMA ZA SHIRIKA
03 Oct, 2026
WATUMISHI COASCO TANGA WAASWA KUFANYA KAZI KWA BIDII NA UADILIFU ILI KUIMARISHA HUDUMA ZA SHIRIKA

WATUMISHI COASCO TANGA WAASWA KUFANYA KAZI KWA BIDII NA UADILIFU ILI KUIMARISHA HUDUMA ZA SHIRIKA

Watumishi wa Ofisi ya Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) Mkoa wa Tanga wameaswa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, nidhamu na ushirikiano ili kuimarisha utendaji na kuhakikisha huduma za Shirika zinaendelea kuwa na ubora na tija kwa wadau.

Rai hiyo imetolewa leo, Oktoba 2, 2026, na Mkurugenzi Mkuu wa COASCO, CPA Alphonce Muro, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Ofisi hiyo, ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake katika Ofisi za Mikoa za COASCO kwa lengo la kusikiliza changamoto, maoni na mapendekezo ya watumishi na kuweka hatua za kuboresha zaidi utendaji na huduma za Shirika.

“Kila mmoja wenu aipende COASCO, mfanye kazi kwa nidhamu na uadilifu ili kuboresha utendaji na huduma za Shirika kwa wadau,” amesema CPA Muro.

Aidha, CPA Muro amewasisitiza watumishi kuongeza matumizi ya TEHAMA katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi, kurahisisha utendaji na kuimarisha utoaji wa huduma.

Pia amewataka kila mtumishi kuibeba kwa vitendo kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu”, kwa kuzingatia kuwa uadilifu ni msingi muhimu wa kuimarisha utawala na maendeleo ya sekta ya ushirika.

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Mkoa wa COASCO Tanga, CPA Philipo Masasi, amesema watumishi wataendelea kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha Vyama vyote vya Ushirika vilivyopo Mkoa wa Tanga vinakaguliwa, huku wakifuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi kwa lengo la kuhakikisha yanasaidia kuleta maboresho katika vyama hivyo.