COASCO YAWANOA VIONGOZI, WATENDAJI WA VYAMA VYA USHIRIKA KUIMARISHA UTAWALA NA UENDESHAJI
COASCO YAWANOA VIONGOZI, WATENDAJI WA VYAMA VYA USHIRIKA KUIMARISHA UTAWALA NA UENDESHAJI
Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limewajengea uwezo viongozi na watendaji wa Vyama vya Ushirika katika uhasibu, ukaguzi wa ndani, TEHAMA na masuala ya kodi, kwa lengo la kuimarisha usimamizi na ulinzi wa rasilimali za wanachama na kuboresha uendeshaji wa Vyama hivyo
Akifungua mafunzo hayo leo, Septemba 23, 2026, katika Ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa COASCO, CPA Alphonce Muro, amesema mafunzo hayo yamejikita katika maeneo muhimu yanayogusa moja kwa moja mifumo ya usimamizi, uwajibikaji na utendaji wa Vyama hivyo.
“Mafunzo haya yamebeba mada muhimu zikiwemo uwasilishaji na ufafanuzi wa taarifa za fedha kwa kuzingatia IFRS 18, masuala ya kodi na Sheria ya Fedha ya mwaka 2026, masuala ya ESG, misingi muhimu ya ukaguzi wa ndani, utayarishaji wa taarifa za fedha za mwisho wa mwaka pamoja na usalama wa mtandao na faragha ya taarifa,” amesema CPA Muro.
Aidha, CPA Muro amewaelekeza washiriki kuzingatia mambo matano baada ya mafunzo hayo, ambayo ni kuandaa mpango wa utekelezaji, kuwashirikisha wengine watakaporudi katika vyama vyao, kupitia mifumo muhimu, kufanyia kazi hoja zinazojirudia na kupima matokeo ya mafunzo hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri na Tafiti wa COASCO, CPA Golden Kajaba, amesema mafunzo hayo ya siku tatu yamewakutanisha viongozi na watendaji wa Vyama vya Ushirika kwa ajili ya kuboresha uendeshaji wa Vyama hivyo.
Naye CPA Hilda Loishiye kutoka Bima ya Afya SACCOS, kwa niaba ya washiriki, amesema mafunzo hayo yamewasaidia kuongeza uelewa katika usimamizi wa fedha, uzingatiaji wa matakwa ya kisheria na matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali, huku akieleza kuwa watatumia maarifa waliyoyapata kuboresha utendaji katika vyama vyao
