Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO)

COASO Logo
COASCO YAISISITIZA MDD SACCOS KUIMARISHA UTAWALA BORA NA USIMAMIZI WA FEDHA
20 Oct, 2026
COASCO YAISISITIZA MDD SACCOS KUIMARISHA UTAWALA BORA NA USIMAMIZI WA FEDHA

COASCO YAISISITIZA MDD SACCOS KUIMARISHA UTAWALA BORA NA USIMAMIZI WA FEDHA

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limesisitiza umuhimu wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Madaktari (MDD SACCOS LTD) kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa fedha ili kulinda rasilimali za wanachama na kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa Chama hicho.

Msisitizo huo umetolewa Octoba 17, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa COASCO, CPA Alphonce Muro, alipokuwa akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Tisa wa Chama hicho, uliofanyika katika jengo la OSHA jijini Dodoma ambapo amesema viongozi wa Chama hicho wanapaswa kuweka mbele maslahi ya Wanachama. ”Simamieni uwazi wa taarifa za fedha, shughulikieni hoja za ukaguzi na epukeni upendeleo katika huduma za mikopo, heshima ya uongozi hujengwa na manufaa ambayo wanachama wanayaona” amesema CPA Muro

Ameongeza kuwa matokeo ya ukaguzi yanapaswa kutumika kama msingi wa kuboresha uendeshaji wa Chama na kuimarisha imani ya wanachama.

CPA Muro, amesema COASCO iko tayari kushirikiana na MDD SACCOS katika maeneo ya ukaguzi, mafunzo na ushauri wa kitaalam kuhusu utawala bora, usimamizi wa fedha, udhibiti wa ndani na usimamizi wa vihatarishi, kwa kuzingatia majukumu na taratibu zinazotumika.

Kwa upande wake , Mwenyekiti wa Bodi ya SACCOS hiyo, Godbless Mbua, amesisitiza kuendelea kuweka jitihada katika uimarisha uendeshaji wa SACCOS hiyo pamoja na kuboresha huduma kwa wanachama na kulinda rasilimali zao.

Aidha, Chama hicho kimepokea na kujadili Taarifa ya Ukaguzi na taarifa za fedha kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 31/12/2025 zilizowasilishwa na Mkaguzi kutoka Ofisi ya COASCO Mkoa wa Dodoma, Rehema Omar