Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO)

COASO Logo
CPA MURO: UBORA NA MATOKEO YA UKAGUZI NI KIPAUMBELE CHA COASCO
23 Sep, 2026
CPA MURO: UBORA NA MATOKEO YA UKAGUZI NI KIPAUMBELE CHA COASCO

CPA MURO: UBORA NA MATOKEO YA UKAGUZI NI KIPAUMBELE CHA COASCO

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), CPA Alphonce Muro, amewataka watumishi wa Ofisi ya Mkoa wa Arusha kuzingatia ubora wa ukaguzi na kuhakikisha mapendekezo ya ukaguzi yanasaidia kuboresha uwajibikaji na utawala bora wa Vyama vya Ushirika.

CPA Muro ametoa rai hiyo leo, Septemba 21, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Ofisi ya COASCO Mkoa wa Arusha, ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake katika Ofisi za Mikoa za Shirika, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha Vyama vyote vya Ushirika vilivyopo katika Mikoa ya Arusha na Manyara vinakaguliwa kikamilifu.

“Tuhame kutoka kwenye kuhesabu idadi ya Vyama vya Ushirika vilivyokaguliwa kwenda kwenye ubora wa ukaguzi na ukaguzi wenye matokeo, na hicho ndicho kipaumbele changu namba moja,” amesema CPA Muro.

Amesema ukaguzi unapaswa kwenda zaidi ya kubaini changamoto, bali kutoa mapendekezo yenye ubora na yanayotekelezeka ili kusaidia vyama hivyo kuongeza uwajibikaji.

Aidha, CPA Muro amewataka watumishi kuzingatia uadilifu, kutunza siri za kikazi, kufanya kazi kwa nidhamu na kuhakikisha majukumu yanakamilishwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Ushirika wa Mkoa wa Arusha, Peter Lema, kwa niaba ya watumishi wa Mkoa huo, amesema wamejipanga kutoa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza mipango na malengo ya COASCO kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya sekta ya ushirika nchini.