Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO)

COASO Logo
CPA MURO: UBORA WA UKAGUZI CHACHU YA MABORESHO YA VYAMA VYA USHIRIKA KILIMANJARO
03 Oct, 2026
CPA MURO: UBORA WA UKAGUZI CHACHU YA MABORESHO YA VYAMA VYA USHIRIKA KILIMANJARO

CPA MURO: UBORA WA UKAGUZI CHACHU YA MABORESHO YA VYAMA VYA USHIRIKA KILIMANJARO

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), CPA Alphonce Muro, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ubora wa ukaguzi ili kuhakikisha matokeo na mapendekezo ya ukaguzi yanachochea maboresho yenye tija katika Vyama vya Ushirika vya Mkoa wa Kilimanjaro

CPA Muro amesema hayo Oktoba 1, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi katika ofisi hiyo, ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake katika Ofisi za Mikoa za Shirika kwa lengo la kusikiliza changamoto, maoni na mapendekezo ya watumishi na kuboresha zaidi utendaji na huduma za Shirika.

Amesema ukaguzi unapaswa kuleta tija kwenye Vyama vya Ushirika, ulete mabadiliko na kuboresha uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za Vyama hivyo.

Aidha, CPA Muro amesisitiza umuhimu wa Shirika hilo kuendelea kutoa huduma za ushauri wa kitaalam na mafunzo kwa viongozi na watendaji wa Vyama vya Ushirika, ili kuwawezesha kupata maarifa na uwezo unaohitajika katika kuimarisha utendaji na uendeshaji wa vyama.

Katika ziara hiyo, CPA Muro amewataka watumishi kudumisha bidii, uadilifu, nidhamu ya muda na ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao.

Naye, Mkaguzi Mwandamizi wa COASCO, Loice Chege, kwa niaba ya watumishi, amemshukuru Mkurugenzi Mkuu kwa kutembelea ofisi hiyo na kusikiliza changamoto, maoni na mapendekezo yao, huku akiahidi kuwa watumishi wataendelea kufanya kazi kwa bidii na kutoa ushirikiano katika kutekeleza majukumu na kuimarisha huduma za Shirika.