CPA MURO AANZA ZIARA ZA OFISI ZA MIKOA YA COASCO, ASISITIZA UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA KWA ASILIMIA 100
CPA MURO AANZA ZIARA ZA OFISI ZA MIKOA YA COASCO, ASISITIZA UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA KWA ASILIMIA 100
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), CPA Alphonce Muro, amefanya ziara ya kikazi ya kwanza katika Ofisi ya Mkoa ya Shirika jijini Dar es Salaam na kusisitiza Vyama vya Ushirika vilivyopo Dar es Salaam na Pwani kukaguliwa kwa asilimia 100 ili kuongeza uwajibikaji katika vyama hivyo.
CPA Muro ameyasema hayo leo, Septemba 12, 2026, wakati wa ziara yake katika Ofisi ya Mkoa ya COASCO Dar es Salaam, ikiwa ni ziara yake ya kwanza katika ofisi za mikoa za Shirika tangu kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu.
Katika ziara hiyo, pia ametembelea nyumba za makazi zinazomilikiwa na Shirika zilizopo Chang’ombe na Mtaa wa Mazengo, Upanga, jijini Dar es Salaam. Katika ziara hiyo, CPA Muro amekutana na watumishi wa ofisi hiyo na kusikiliza changamoto, maoni na mapendekezi yao kwa lengo la kuboresha utendaji na ubora wa huduma za Shirika.
“Tuhakikishe tunakagua Vyama vya Ushirika vya Kifedha na vya mazao kwa asilimia 100 vilivyopo katika maeneo ya Dar es Salaam na Pwani ili kuzidi kuimarisha uwajibikaji katika vyama hivyo,” amesema CPA Muro. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kufanya ukaguzi wenye ubora na unaoleta matokeo, pamoja na kuhakikisha taarifa za ukaguzi zinakuwa na mapendekezo bora na yanayotekelezeka.
Kwa upande wake,Mkaguzi wa Ofisi hiyo, CPA Michael Makundi, kwa niaba ya watumishi, amemshukuru Mkurugenzi Mkuu kwa kufanya kikao hicho kilichowapa nafasi ya kueleza kero, changamoto na maoni yao kwa ajili ya kuboresha utendaji wa Shirika.
