CPA MURO: MAGEUZI YA KIUTENDAJI NGUZO YA KUIMARISHA HUDUMA ZA COASCO
CPA MURO: MAGEUZI YA KIUTENDAJI NGUZO YA KUIMARISHA HUDUMA ZA COASCO
Watumishi wa Ofisi ya Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) Mkoa wa Morogoro, wameaswa kufanya mageuzi ya kiutendaji na kimtazamo, huku wakizingatia uwajibikaji na uadilifu ili kuimarisha zaidi ubora wa huduma za Shirika.
Rai hiyo imetolewa leo, Septemba 14, 2026, na Mkurugenzi Mkuu wa COASCO, CPA Alphonce Muro, wakati wa mwendelezo wa ziara yake katika Ofisi za Mikoa za Shirika, ambapo ametembelea Ofisi ya COASCO Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kusikiliza changamoto na maoni ya watumishi hao ili kuboresha utendaji na ubora wa huduma za Shirika.
CPA Muro amesema kila mtumishi anapaswa kubadili utamaduni wa kiutendaji na kuufanya kuwa chachu ya kuongeza ubora wa huduma za ukaguzi, ushauri wa kitaalam, tafiti, uchunguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika na taasisi nyingine.
Aidha, amesisitiza watumishi kufanya kazi kwa uadilifu, kushirikiana na kuwajibika kikamilifu katika majukumu yao ili kuchochea utawala bora katika vyama vya ushirika.
Katika ziara hiyo, CPA Muro amehimiza Ofisi hiyo kuhakikisha Vyama vyote vya Ushirika vilivyopo Mkoa wa Morogoro vinakaguliwa.
Kwa upande wake, Jerad Lwitiko, aliyemwakilisha Mkaguzi wa Mkoa, kwa niaba ya watumishi wenzake, ameahidi ushirikiano wa dhati, uwajibikaji na kujituma katika kutekeleza majukumu yao.
