Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO)

COASO Logo
CPA MURO AWEKA MWELEKEO MPYA WA COASCO KUPITIA VIPAUMBELE SABA
04 Sep, 2026
CPA MURO AWEKA MWELEKEO MPYA WA COASCO KUPITIA VIPAUMBELE SABA

CPA MURO AWEKA MWELEKEO MPYA WA COASCO KUPITIA VIPAUMBELE SABA

Katika kikao chake cha kwanza na watumishi wa Shirika tangu kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), CPA Alphonce Muro amebainisha vipaumbele saba vya kuimarisha utendaji wa Shirika na kuboresha huduma zake kwa wadau

Vipaumbele hivyo ni kuimarisha ubora wa ukaguzi, kuhakikisha COASCO inakuwa kitovu cha utafiti na maarifa, kuongeza matumizi ya teknolojia, kuimarisha mazingira na uwezo wa watumishi, kujenga mahusiano ya kimkakati na taswira chanya ya Shirika, kuimarisha uwezo endelevu wa kifedha pamoja na kujenga utamaduni bora wa kiutendaji.

CPA Muro amebainisha hayo leo, Septemba 3, 2026, katika kikao na watumishi wa Shirika kilichofanyika Ofisi ya Makao Makuu ya Shirika, Dodoma, huku watumishi kutoka mikoani wakishiriki kwa njia ya mtandao. 

Katika Kikao hicho CPA Muro, amesema vipaumbele hivyo vitakuwa msingi wa kuleta mageuzi katika utendaji wa Shirika na kuboresha huduma zake kwa wadau.

Aidha, amesisitiza watumishi kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji, uadilifu na ubunifu, huku akitambua mchango wao katika mafanikio ya Shirika na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa COASCO, CPA Jeremiah Mugeta, amesema kila mtumishi ana nafasi muhimu katika mafanikio ya Shirika na kuwataka kuendelea kushirikiana ili kufikia malengo yaliyowekwa.