MKUU WA WILAYA YA KIBAHA AHIMIZA BODI NA WATENDAJI WA VYAMA VYA USHIRIKA KUTUMIA MAFUNZO YA COASCO KAMA CHACHU YA MATOKEO CHANYA
MKUU WA WILAYA YA KIBAHA AHIMIZA BODI NA WATENDAJI WA VYAMA VYA USHIRIKA KUTUMIA MAFUNZO YA COASCO KAMA CHACHU YA MATOKEO CHANYA
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simoni, amezihimiza bodi na watendaji wa vyama vya ushirika kutumia mafunzo ya uhasibu, TEHAMA na kodi yanayotolewa na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) kama chachu ya kuimarisha uwajibikaji, utawala bora na utamaduni wa matokeo chanya katika uendeshaji wa vyama hivyo.
Amesema hayo leo, Juni 17, 2026 wakati akifungua mafunzo ya siku tatu yanayofanyika katika Ukumbi wa Destiny, Kibaha. Amesema mafunzo hayo yamebeba mada muhimu zitakazosaidia kuimarisha utendaji na usimamizi wa vyama vya ushirika.
“Viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika ninawahimiza mzingatie mafunzo haya yatakayowasaidia kuviendesha vyama vyenu kwa weledi, uwazi na uwajibikaji, pamoja na kujenga utamaduni wa matokeo chanya katika uendeshaji wa vyama vyenu,” amesema Mhe. Simoni.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Ushauri wa Biashara wa COASCO, CPA Anna Thomas Shao, amesema mafunzo hayo yanayofanyika kuanzia Juni 17 hadi 19, 2026 yamebeba mada mbalimbali zenye tija ikiwemo uongozi, uandaaji wa taarifa za fedha za mwisho wa mwaka kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uhasibu, kodi, matumizi ya TEHAMA.
Naye Mtendaji Mkuu wa Viwango SACCOS, CPA Khalid Massawe, kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, amesema mafunzo hayo yatachangia kuongeza ufanisi katika utendaji, utunzaji wa kumbukumbu na uendeshaji wa vyama hivyo.
