Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO)

COASO Logo
TCDC, COASCO ZAWEKA MWELEKEO MPYA WA USIMAMIZI NA UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA
19 Jul, 2026
TCDC, COASCO ZAWEKA MWELEKEO MPYA WA USIMAMIZI NA UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA

TCDC, COASCO ZAWEKA MWELEKEO MPYA WA USIMAMIZI NA UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA

Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), kwa kushirikiana na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), zimeweka mwelekeo mpya wa kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa vyama vya ushirika nchini kwa lengo la kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika sekta ya ushirika.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Julai 9, 2026, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson O. Ndiege, katika Ukumbi wa Corridor Spring, Arusha amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Daniel G. Chongolo, Waziri wa Kilimo ya kuendelea kuimarisha sekta ya ushirika.

“Mwelekeo huu utawezesha taasisi zetu kufanya kazi kwa uratibu zaidi, kutumia taarifa sahihi katika kufanya maamuzi na kuongeza uwajibikaji katika usimamizi wa vyama vya ushirika kwa manufaa ya wanachama na Taifa kwa ujumla,” amesema Dkt. Ndiege.

Dkt. Ndiege amesema TCDC na COASCO zimekubaliana kuunganisha mifumo ya MUVU na COADMIS, kuimarisha uratibu wa shughuli za ukaguzi, kutumia takwimu za pamoja na kuendelea kujenga uwezo wa viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika.Pia, taasisi hizo zitasimamia utekelezaji wa kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu” ili kuimarisha uwazi na maadili katika sekta ya ushirika.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COASCO, CPA Jeremiah Mugeta, amesema COASCO itaendelea kushirikiana kwa karibu na TCDC kuhakikisha mifumo ya usimamizi na ukaguzi inaunganishwa, matumizi ya TEHAMA yanaimarishwa na huduma zinazotolewa kwa vyama vya ushirika zinaendelea kuwa bora, zenye uwazi na zenye kuleta matokeo chanya kwa wanachama na Taifa.

Vilevile, CPA Mugeta ameelekeza kuwa ukaguzi wa Vyama vya Ushirika utaanza tarehe 20 Julai, 2026. Hivyo, ameviomba vyama vyote ambavyo muda wa ukaguzi wake umefika kuwasilisha taarifa za fedha kwa ajili ya ukaguzi huo.